Header Ads

ad

USHUPAVU NI MSINGI WA KUYAMUDU MAZINGIRA NA KICHOCHEO CHA MAENDELEO YETU NA JAMII YETU.

Picha ya Fred Matuja
Eric Robert Greitens ni gavana wa 56 wa jimbo la Missouri nchi Marekani. Atakuwa anatimiza miaka 42 ifikapo April 10 mwaka huu.
Pamoja na kuingia katika shughuli za kisiasa na uongozi, pia Eric ni afisa wa kijeshi mwenye cheo (rank) cha luteni kamanda na kwa mfumo wa nchi za majeshi wa Commonwealth ambayo na Tanzania ni mwanachama, luteni kamanda ana cheo cha meja.
Gavana Eric Greitens alimshirikisha mwandishi wa kitabu aitwae Bill Murphy; Bill kaandika kitabu chenye dondoo kwa wazazi na walezi namna ya kutengeneza mfumo wa malezi ya watoto na vijana wenye mafanikio (How to Raise Successful Kids).
Katika kitabu hicho, Eric katoa mbinu kadhaa za kukuza akili ya mtoto au kijana ili afanikiwe maishani kwa kuwa na mchango wa maendeleo katika jamii yake pia. Binafsi kama Mtanzania niliepata kusoma taaluma ya elimu (au ualimu kama ambavyo watu wengi wamezoea kuita) nimeguswa na maarifa haya ni ninawiwa deni la kumshirikisha mtu yeyote kupitia ukurasa huu kwa lengo la kuchukua maarifa haya na kuyatumia yeye binafsi hali kadhalika kusaidia watoto na vijana walio nyumbani kwako na katika jamii inayotuzunguka kwa ujumla ili tuwe na Taifa lenye kuwajibika kupigana kwa lengo la kufanikiwa na kuambukiza mafanikio kwa wengine.
Pamoja na mfumo wa utandawazi na mabadiliko ya kimfumo hapa nchini, ila bado msingi wa ujamaa una sehemu kubwa sana Tanzania. Mfano, kama kuna msiba au harusi mfumo wa michango kufanikisha hafla hizi una misingi ya kijamaa. Katika mfumo wa kibepari hawana mifumo ya kusaidiana kama ilivyo hapa Tanzania ya leo. Hivyo kama wajamaa, tuna mengi ya kukumbatia na kuelimishana hususani, nyakati hizi zenye changamoto kubwa za kimtazamo. Pamoja na changamoto hizi za kifikra ambapo taarifa zinasafiri kutoka pande yoyote ya dunia kwa teknolojia ya mawasiliano, bado tuna jukumu la kuweka misingi ya kizalendo yenye kusudi jema la kutafsiri dhana ya kuwajibika ili kuijenga Tanzania yetu. Taifa hili ni letu, watu wa taifa hili ni ndugu zetu, tunawajibika kuwajenga kwa pamoja ili tuwe taifa lenye mafanikio yanayotufaidisha wote.
Luteni kamanda Eric anatufundisha, moja ya msingi wa mafanikio kwa mtoto, kijana na mtu yeyote maishani ni USTAHIMIVU (resiliance). Tafsiri rahisi ya ustahimivu ni uwezo wa kurejea kwa haraka kutoka katika changamoto za magumu; au hali ngumu na kuendelea kuwa na mzalishaji mwenye tija. (being productive and effective)
Ukisoma maisha ya yeyote aliefanikiwa na kuacha alama katika jamii yake, utakuta kila moja alikuwa na sifa hii. Eric amesisitiza, Inahitaji kuvumilia ili kufanikiwa hususani katika umahiri katika jeshi la Marekani. Nina hakika, nidhamu hii itakuwa inagusa na majeshi mengine yote hapa duniani. Hali kadhalika nidhamu kama hii inagusa watu waliofanikiwa iwe katika taaluma, biashara, harakati kama za kupigania uhuru walizofanya akina Mwl. Nyerere na kadhalika.
Luteni kamanda Eric anasisitiza umuhimu wa kuwasaidia watoto na vijana kwa kuwajengea mifumo ya kuwajibika ili kutimiza kusudi la wao kuwepo pale walipo. Ikiwa ni shule, chuoni au kazini, kuna ulazima kila mtu awe na fikra za kutimiza “mission” yay eye kuwa pale yenye mchango endelevu wka jamii yake.
Anasisitiza kuwa, watoto na vijana wanaweza kujifunza kupitia mbinu hizi hali kadhalika mtu yeyote vilevile anaweza kukuza au kuongeza ushupavu wa akili yake ili awe na ufanisi na tija katika shughuli zake za kila siku.
Kwa muhtasari, hizi ni dondoo chache zilizoainishwa na luteni kamanda Eric, ambazo sisi wazazi, walezi, viongozi katika maeneo ya kazi tunaweza kufanya ili kuleta kichocheo cha kuathiri watu walio tuzunguka,
1. Weka mfano mkuu wa kuigwa (Set a great example)
Kama ilivyo program yoyote ile yenye nia ya kuboresha maisha ya mtu, kuongeza ushupavu kunahitaji kuonesha hali ya kujitoa (demonstrating commitment). Mzazi, mlezi ambae una nafasi ya uongozi kwa watoto na vijana una wajibu wa kuwatia moyo watoto, vijana na watu wegine wanaokuzunguka kwa kujifunza kwa mfano kwa namna wewe unavyo ishi na kutenda kazi zako.
Kutoa tafsiri nzuri ili ieleweke, kumbuka msemo wa Ralph Waldo Emerson… “maisha yetu tunayoishi yanasema sauti kubwa sana kuliko yale tunayotamka”
"Watu wakiona jinsi unavyoweza kujinyanyua pale unapobamizwa chini, watajifunza tabia hiyo kwa kuiga toka ndani ya mioyo yao”
2. Wajibika/ Timiza wajibu wako (Take responsibility)
Kuwajibika maana yake ni unahusika kudhibiti maisha yako. Kuna mambo utatambua huwezi kuyadhibiti, na ukifahamu tofauti, utacheza nafasi yako kwa kufanya kila uwezalo kwa lile lililo ndani ya uwezo wako ili ufanikiwe.
Tunawajibika kuwafundisha watoto na vijana, hali kadhalika nasi kuishi maisha ya kutowalaumu au kutafuta sababu, ila kuwajibika kimatendo kwa mambo yanayotuhusu sisi, familia na jamii zetu.
3. Tafuta kuwatumikia wengine (Seek to serve others)
Pamoja na kutengeneza mfumo wa kuwajenga wengine ili kuwa na mchango kwao na dunia inayokuzunguka (kuwa na athari chanya kwa watu wengine). Toa huduma kwa wegine, maisha si kwa ajili wewe peke yako. Kila mmoja anawajibika kuwa rasimali na utambulike kama mtu wa kutegemewa na jamii yako kama suluhisho kwa changamoto zinazoizunguka jamii.’
Eric anasema "Watu tunatakiwa kujua tuna kitu cha kuwapa wengine” na tunawajibu wa kijifunza kutoa taswira ya kubadili mazingira yanayotuzunguka kuwa bora zaidi.
4. Tujifunze kushukuru kila siku (Practice daily gratitude)
Tabia ya kushukuru iko kwa watu wengi waliofanikiwa. Watu wanaotaka kufanikiwa na waliofanikiwa mara kwa mara hufanya majukumu yao bila kijali wanapitia changamoto gani. Hupenda kujenga tabia ya kuwashukuru wengine. Ili kunapanua uwezo wako wa kutenda kazi kama kiongozi (mzazi, mlezi una wajibu wa kuonesha uongozi) kwa kujenga akili yako kujikubali na kushukuru Mungu kwa vipawa, karama na uwezo ulio nao ambao umejaliwa kwa ajili ya kuwasaidia watu walio katika mzunguko wako wa ushawishi.
Tunawajibika kukabiliana na kila siku kwa shauku ya kufanikisha majukumu yetu; hata siku mbaya ya kukatisha tamaa na yenye hali ngumu, jione una kitu bora pengine kuliko wengine katika jamii iliyokuzunguka, na jiweke/jione una mchango kwa dunia inayokuzunguka.
Itaendelea
Fredrick Matuja
fmatuja@hotmail.com(P.T)