Header Ads

ad

SIMULIZI ZA KUSISIMUA.. JE, NI KWELI GENERAL IDD AMIN ALIMUUA MKEWE?

Ndugu zangu,
AMA kwa hakika, wanawake ni moja ya sura za Idd Amin ambazo hazikujulikana sana nje ya mipaka ya Uganda.
Inasemwa, kuwa General Amin alikuwa anahusudu sana wanawake. Kwamba alikuwa tayari kuua kwa sababu ya mwanamke.
Ikafika wakati, General Idd Amin alikatisha ziara au shughuli ya Kiserikali ili apate fursa ya kwenda kufanya ngono na mwanamke.
Walinzi wake wa karibu walifanya kazi pia ya kwenda kuwachukua wanawake aliowatamani bosi wao.
Walinzi hao walikuwa na kibarua pia cha kukariri ni nani bibi wa bosi wao, maana vimada wa Idi Amin walikuwa wengi.
Walinzi hao walifanya kazi pia ya kukariri ni nani mtoto wa Amin , maana, idadi ya watoto wa Amin waliotambulishwa kwa watu wa usalama wa Amin ilikuwa kubwa.
Inasemwa pia, kuwa kifo cha mmoja wa wake wa General Amin aitwaye Kay, kilitokana na ajali ya gari, ni ajali ya kushangaza. Ni ya kupangwa.
Hadi hii leo kuna wanaoamini ajali hiyo haikuwa kazi ya Mungu bali kazi ya General Idd Amin aliyoipanga vema kwa kushirikiana na watu wake wa usalama.
Hata hivyo, hakuna aliyeweza kuthibitisha ukweli mzima juu ya jambo hilo.
Tukio lingine la kushangaza katika mauhusiano ya General Idd Amin na wake zake ni pale alipotoa talaka kwa mpigo kwa wake zake watatu.
Wake zake hao ni Malyamu , Nora na Kay. Amin aliwatuhumu Malyamu na Nora kwa kujihusisha na masuala ya biashara wakiwa ndani ya ndoa. Kay naye alipewa talaka kwa kile ambacho Idi Amin alidai ni binamu yake!
Lakini, ukweli juu ya kuharibika kwa mahusiano hayo ya ndoa kati ya General Idd Amin na wake zake hao ni kwa Amin mwenyewe kuendekeza zaidi wanawake wa nje na kuwasahau wake zake wa ndoa.
Jambo hilo linathibitishwa pia na mwandishi Henry Kyemba ambaye nimebahatika kusoma kitabu chake kiitwacho; ' State Of Blood'.
Inasemwa, kuwa kitendo cha General Idd Amin kuwaacha wake zake hao na kutumia muda mwingi kulala na wanawake wa nje kuliwafanya wake zake hao, nao kujisikia kutotimiziwa mahitaji yao ya ndani ya ndoa. Nao walianza kutafuta mabwana wa nje.
Na hakika, siku ile ya wake hao kupewa talaka zao walifurahia sana. Walijisikia wako huru kufanya mambo yao nje ya nyumba ya General Idd Amin.
Ndoa yao na Amin ilikuwa ni kama kifungo.
Hawakupenda kuwa na mahusiano ya siri na mabwana wa nje.
Siku hiyo ya kupewa talaka kwa mpigo, Malyamu, Nora na Kay walifanya sherehe kubwa.
Kusheherekea kuachwa na General Idd Amin. Katika sherehe hiyo waliwakaribisha mabwana zao. General Idd Amin hakupewa mwaliko! Walimwambia abaki na mkewe kipenzi , Madina.
Hata hivyo, Malyamu, Nora na Kay walijikuta katika wakati mgumu nje ya ndoa ya Amin. Mikasa gani iliwafika?
Maggid,
Iringa.