Header Ads

ad

MAMBO 8 UTAKAYOJUTIA KUTOFANYA UKIWA NA UMRI WA MIAKA KATI YA 20 NA 30 KATIKA MAISHA YAKO

MAMBO 8 UTAKAYOJUTIA KUTOFANYA UKIWA UMRI WA MIAKA KATI YA 20 NA 30Muda unaoutumia wakati wa miaka ya ishirini inawezekana kabisa ndio wakati wa muhimu sana kwenye maendeleo yako binafsi. Maana ni wakati ambao wengi ndio huanza biashara na wengine ndio huwa na ndoto za kuwa wajasiriamali siku moja au wengine ndio huwa wanazijenga taaluma zao, lakini lipo tatizo, je ni lipi?, hakuna muongozo wowote ulioandaliwa kwa ajili ya kuwaongoza vijana kwenye wakati huu muafaka hivyo wengi huishia kujuta baadae kwa kushindwa kufanya mambo sahihi kwa wakati sahihi. Tuangalie mambo 8 utakayojutia kutoyafanya ukiwa umri wa miaka kati ya 20 na 30.

Kutong’ang’ana mambo yanapokuwa magumu; maisha hayajawahi na hayatawahi kuwa marahisi kama wengi wanavyodhani hivyo unahitaji kung’ang’ana kama unataka kufika mbali. Usiwe mtu wa kukata tamaa mapema, ukifeli  mara moja haina maana utafeli milele, chukulia kufeli kama sehemu ya kujifunza, ili ufanikiwe unatakiwa uwe mtu mwenye moyo na akili imara.

Kutojaribu jambo jipya/tofauti; wengi hatupendi kujaribu mambo mapya kwasababu tunaogopa kufeli na tunataka tuwe na uhakika kwanza na hasa linapokuja suala la biashara au ujasiriamali. Tunashindwa kuelewa kwamba kila jambo tunalolifanya halina uhakika sana, mfano ukioa upo uwezekano wa kuachana, ukienda shule upo uwezekano wa kufeli, ukilala unaweza usiamke n.k. Iweje linapokuja suala la kajaribu jambo jipya kama biashara au ujasiriamali uogope kufanya, lakini ukweli ni kuwa ili uweze kufanikiwa kwenye maisha ni lazima ujaribu kufanya jambo jipya na maisha yako, na inakuwa ni rahisi zaidi ukiyafanya haya ukiwa bado kijana.

Kutoweka akiba;  ni muhimu sana kuanza kuwa na tabia ya kujiwekea akiba toka ukiwa kijana hata kamani kidogo kiasi gani angalau mara moja kila mwezi. Tabia hii itakusaidia kuwa na nidhamu hata pale utakapopata nafasi ya kuwa na kipato kikubwa, wanasema ukiweza kuwa na nidhamu ukiwa na kidogo hata kikubwa kikija nidhamu itakuwa palepale. Ukifanya hivi mapema inakujengea mazingira mazuri ya utu uzima wako, tukumbuke pia kadiri umri unavyokwenda majukumu nayo huwa yanaongezeka zikiwemo na changamoto za kiafya pia. Kumbuka kuweka akiba kabla ya kutumia, sio utumie kwanza ndio kinachobaki kiwe akiba.

Kutofanya uchunguzi kabla ya kuwekeza; kila mmoja atakwambia uanze kuwekeza toka ukiwa kijana mdogo, wengine watakwambia jaribu ujasiriamali, wazazi watakwambia nunua kiwanja uanze kujenga, maafiki zako watakushauri ununue gari lako la kwanza. Wakati huu washauri huwa ni wengi sana, lakini ukweli ni kwamba usiwekeze muda na pesa yako mahali ambapo hujafanya uchunguzi vya kutosha, usifanye kitu kisa fulani anafanya. Usinunue gari kisa rafiki zako au wafanyakazi wenzako wote wana magari, fanya maamuzi baada ya utafiti na kuona ni kwa kiasi gani kitu hiko kitakufaidisha sasa na baadae

Kutofanya mazoezi; kawaida mwili wa mwanadamu huanza kubadilika kadiri umri unavyokwenda, vivyo hivyo ukakamavu wa mwili wako na nguvu za misuli hupungua kulingana na umri unavyoenda ndio maana watu wengi hunenepa sana kati ya miaka 30 na 45. Ili usikumbane na changamoto kubwa za kiafya ni vizuri kuanza kufanya mazoezi katika umri mdogo ili uwe na mwili imara kuendana na umri wako.

Kupoteza mahusiano na watu wa maana; watu wa maana ni wapi?, ni watu ambao labda umesoma nao, mmefanya kazi pamoja, n.k., lakini ni wale watu ambao mnafahamiana na kuelewana vizuri. Sasa jambo baya kabisa ni kupoteza uhusiano na watu kama hawa kwenye maisha yako, sio kwa sababu umepata kazi mpya basi utafute marafiki wapya, lakini pia sio sababu biashara yako haikufanikiwa basi uachane na watu waliokusaidia kimawazo wakati inaanza. Kumbuka pia kila unaekutana nae kwenye maisha una umuhimu wake kwa njia moja au nyingine, hata watu wabaya wana umuhimu wake kwa sababu watakupa mafunzo ya jinsi ya kuishi na watu wa aina hiyo pindi utakapokutana nao tena.

Kutokuwa na nidhamu; kuwa na nidhamu haiishii pale unapo achana na wazazi wako au pale unapomaliza masomo yako., nidhamu ni suala la kuliangalia katika kipindi chote cha maisha yako. Lazima uwe na nidhamu katika mambo yako yote, kama ni biashara basi utenge biashara na mambo yako ya kijamii au urafiki, nidhamu inahitajika ili uweze kuyafikia malengo yako ya muda mrefu. Unahitaji kuwa na nidhamu na pesa zako, nidhamu na afya yako, nidhamu kwenye mahusiano yako, n.k. kwa ufupi nidhamu inahitajika kwenye mambo yako yote. Gharama utakayolipa sasa kuwa na nidhamu ni ndogo sana kulinganisha na gharama utakayolipa baadae. Nidhamu ni kufanya yale unayotakiwa kuafanya hata kama hujisikii tena kufanya.

Kutokuwa na uhakika na kile unachotaka kufanya kwenye maisha yako; kugundua kuwa unatakiwa kufanya nini na maisha yako si suala rahisi kama wengi wanavyofikiri na kinachosikitisha zaidi ni kitu ambacho hutakaa ufundishwe shuleni au hata mahali unaposali. Hivyo ni jukumu lako binafsi kujua unataka nini na unataka baadae yako iweje, na inakuwa rahisi zaidi kutambua hili ukiwa na umri mdogo kwa sababu ni watu wazima wachache sana wanaojua wameumbwa kufanya nini na maisha yao. Mpaka utambue sababu ya maisha yako ndipo utakapo yafurahia maisha, na ili uweze kutambua sababu ya maisha yako lazima uwe na majibu ya maswali matano ya moyo wa mwanadamu. Maswali hayo ni, Mimi ni nani?, Je nimetokea wapi?, Nipo hapa kufanya nini?, Nini ninaweza kufanya?, na Je ninaelekea?. Hakika ukiwa na majibu sahihi ya maswali haya basi maisha yako yatajaa furaha na amani tele.

Wanasema miaka ya 20 ni miaka ya mipango na miaka ya 30 ni miaka ya utekelezaji, ninachoweza kukusaidia ni kusema kuwa, haijalishi sasa una umri gani na pia haijalishi una maisha ya aina gani sasa, bado hujachelewa ndugu yangu. Bado hujachelewa kwa sababu una uwezo wa kujifunza kutokana na makosa uliyoyafanya huko nyuma na kuweka mipango mipya kulingana na nilichokiandika hapa na kuanza kuona mabadiliko chaya kwenye maisha yako.

Tukutane tena wiki ijayo;

KWA MASWALI NA MAONI;
Anko Sam,
Simu: 0715782872 – SMS/Call/WhatsApp
E-mail: ankosam2014@gmail.com,                                      Facebook: Samson Ndosi